Licha ya viongozi wa Kiafrika kukutana jijini Nairobi kuzungumzia
mikakati ya kupambana na ugaidi, wasiwasi uliopo ni ikiwa kweli Afrika
iko tayari kukabiliana na tatizo hili la kimataifa.
Mkutano wa viongozi wa Afrika juu ya ugaidi jijini Nairobi.
Tarehe 21 Septemba 2013 wanamgambo wa al-Shabaab walilivamia jengo la
maduka la Westgate jijini Nairobi, Kenya, ambako waliwauwa watu zaidi ya
60, huku ikivichukuwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo siku nne
kuukomeshwa mzingiro wa jengo hilo. Mwaka mmoja baadaye, taarifa za
uhakika juu ya namna tukio hilo lilivyotokea - kama vile idadi ya
washiriki na njia zilizotumika - bado hazijapatikana.
Kisha baina ya tarehe 14 na 17 Juni 2014, wanamgambo wakavamia kijiji
cha Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, na tena wakawauwa watu zaidi ya 60. Bila
ya shaka, orodha ya mauaji mengine yenye sura kama hiyo imekuwa
ikiendelea.
Aprili 2014, kundi la Boko Haram liliwateka nyara wasichana 276 kutoka
kijiji cha Chibok, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Hadi
sasa, Boko Haram imeshateka watu wengine kadhaa na huku wengi wa
waliowateka awali wakiwa bado mikononi mwao.
Mwili wa mmoja wa waliouawa kwenye mashambulizi ya Mpeketoni.
Mwanzoni mwa Septemba 2014, viongozi wa Afrika walikutana
jijini Nairobi, Kenya, kuujadili ugaidi, ambapo mwenyeji wao, Rais Uhuru
Kenyatta, aliwaambia wenzake ugaidi Afrika ni uhalisia sasa.
"Ni jambo la kutia wasiwasi barani Afrika hivi leo kuona namna makundi
ya kigaidi yalivyoongezeka kwa idadi na kwa uwezo. Boko Haram inaendelea
kuzitia mashakani sehemu za mataifa ya Nigeria, Chad na Cameroon kwa
mbinu mpya, kama vile kuwateka nyara wasichana 200 hivi karibuni, pia
tuna al-Qaida tawi la Maghreb." Alisema Kenyatta kwenye mkutano huo.
Ugaidi ndio mada yetu leo Mbele ya Meza ya Duara, tukiangalia uzito wa
kitisho hiki, athari zake na, kubwa kuliko yote, uhalisia wake na uwezo
wa bara la Afrika kukabiliana nao. Kaskazini, eneo liitwalo Sahel, kuna
tawi la al-Qaida la Maghreb, magharibi kuna Boko Haram, mashariki kuna
al-Shabaab, na kama alivyosema Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kwenye
mkutano huo wa Nairobi, kitisho hiki kinavuuka makundi moja moja tu, na
kuwa muunganiko wa makundi mengine kadhaa ya kihalifu na kigaidi kwa
pamoja.
"Kitisho hiki kinakuwa changamano zaidi kwa kukuwa kwa mafungamano kati
ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, hasa hasa madawa ya
kulevya na magendo ya silaha, biashara haramu ya binaadamu, na
utakatishaji fedha zinazopatikana kwa njia haramu."
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Kwa mujibu wa Rais Idriss Deby wa Chad, ambaye ndiye mwenyekiti
wa sasa wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, mkutano huo
wa Nairobi ulizungumzia uwezekano wa kuwa na mfuko wa pamoja kupambana
na ugaidi barani Afrika.
Lakini je, hilo kweli linawezekana? Je, Afrika inaweza kupambana na
ugaidi kwa nguvu na uwezo wake wote, kiwango ambacho inakabiliana na
mengine? Je, mkutano huu wa Nairobi ulikuja wakati tayari umeshachelewa?
Juu ya yote, sababu za ugaidi barani Afrika ni zipi?
Kuchambua mada hii, Mohammed Khelef anaongoza majadiliano kati ya Maggid
Mjengwa, ambaye ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa za Afrika na
mwanaharakati akiwa Iringa, Tanzania; Ally Saleh, ambaye ni
mwanasheria, mwandishi wa habari wa kimataifa na pia mwanaharakati wa
haki za binaadamu, Zanzibar, na Werunga Simiyu, mchambuzi wa masuala ya
usalama kutoka Nakuru, Kenya.